HISTORIA HALISI YA CHIMBUKO LA KARIAKOO
SHORT BACK STORIES
MTAARISHAJI: MBAJI MOHAMMAD
HISTORIA YA SOKO KUU LA KARIAKOO.
Leo nitakujuza historia halisi ya pahali panapoitwa KARIAKOO. Historia ya jina Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.
Neno Kariakoo, asili yake ni neno la Kiingereza ambalo ni ‘Carrier Corps’, likiwa na maana ya kwamba mahala ambapo ndipo inapomalizikia misafara iliyokuwa ikiwasili kutokea nje ya mji, wakati wa utawala wa wajerumani na waiingereza. Misafara hiyo ilihusisha askari pamoja na wapagazi (wabeba mizigo) kwenye vita, ambao walikuwa wakija mjini ili kupelekwa vitani. wajerumani na waingereza wote walipatumia mahala hapo kwa shughuli hiyo.
Sasa, kama ilivyo kwa maneno mengi mengine yaliyotokana na asili ya Kizungu, Waswahili walishindwa kulitamka neno ‘Carrier Corps’ kisawasawa, na hivyo kulitohoa (kulitamka) Kariakoo. kama ilivyokuwa kwa maneno Msasani (Mussa Hassan), marikiti (market) na mengine mengi.
Hapo mwanzoni, soko hasa lilikuwa kule mjini Uhindini, kwenye Barabara ile inayoitwa Market Street mpaka leo.
Nyuma ya barabara hiyo, kuna Msikiti mkubwa wa Kitumbini ambao ndio uliokuwa Msikiti wa Ijumaa siku hizo, pale misikiti mingine yote midogo ilipokuwa ikifungwa kwa ajili ya kusalia swala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Kitumbini. Kwa hali hiyo, Wazungu kama watawala wakaupa mtaa ule jina la Mosque Street, ambalo limedumu mpaka leo.
Kwa sababu ‘mabwana wakubwa’ hawakupenda zogo, ghasia na kelele za raia kule mjini, soko lile la Market Street likahamishiwa Kariakoo mahala lilipo sasa, ili kuwa karibu na maeneo ya walengwa. Soko la Kariakoo lilikuja kujengwa hivi lilivyo sasa, mnamo mwaka 1967-1968, baada ya kuonekana kwamba lile lilokuwapo mwanzo halikidhi haja, kwani mji ulikuwa umepanuka na kuongezeka sana.
B.J. Amuli, mmoja kati ya Watanzania wa mwanzo kabisa kufuzu katika fani ya usanifu majengo aliyesomea kule Israel, ndiye aliyechora mjengo ule mzuri na wa kupendeza mahala hapo, kukiwa na sehemu ya soko la chini ardhini kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na ununuzi wa mazao kwa jumla kwenye minada.
Zamani soko lilikuwa ni moja tu pale Kariakoo ambalo lilikuwa hilo dogo, lilokuwapo mahala ambapo sasa kuna soko kuu kubwa hapakuwa na masoko mawili kama ilivyo sasa.
SOKO LA KARIAKOO 1969
Soko lenyewe lilikuwa limejengwa kwa mbao na kusimamishwa kwa vyuma na juu limeezekwa mabati. Humo ndani mlikuwa na mbao (kwa maana ya sehemu za kufanyia biashara) zilizojengwa kwa saruji na vikalio vya saruji pia. Katikati kulikuwa na njia ndogondogo za kutenganisha kati ya biashara na biashara pamoja na watu kuweza kupita kwenda huku na kule.
Upande wa Kaskazini wa Soko kulikuwa na sehemu ya kuuzia samaki wabichi, waliokuwa wakiingia sokoni hapo kutokea maeneo ya Bagamoyo, Kunduchi, Msasani, Ununio na Mbweni.
Samaki wengine walikuwa wakija kutoka maeneo ya Kigamboni, Kisiju na visiwa vya Kwale na Mafia. Hakukuwa na Soko la Feri wakati huo kama tulivyozoea sasa hivi kupata mahitaji ya samaki kutoka hapo. Miongoni mwa wauzaji wakubwa wa samaki siku hizo sokoni hapo alikuwa ni Mzee Awadh Mohammed, Mohammed Mabosti, Mzee Majee na Tabu bin Tabu. Hawa walikuwa ndio mawakala wakubwa wakipokea samaki hao na kuwauzia watu rejareja na kwa vipande kwenye meza.
Mbele kidogo ya biashara ya samaki wabichi, ilikuwapo ile ya samaki wakavu wa kuchoma au Waswahili huwaita ‘samaki wa manyalia’ au wa kubanika. Hiki kilikuwa ni kitoweo kizuri sana kinapopikwa na tui la nazi na kuliwa na ugali hapa watu pembezo mwa bahari watakuwa wananilelewa. ambapo watu wa kipato cha chini walikikimbilia sana. Mzee Kondo bin Kondo, aliyekuwa mpenzi mkubwa wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ndiye aliyekuwa maarufu sana kwa kuuza samaki wa kubanika, sokoni Kariakoo. Mbele ya mbao za samaki, ilikuwapo biashara nyengine ya kuuza tumbaku au ugoro, ambayo ilichukua eneno kubwa sana la soko; kwani biashara ya ugoro iko ya aina nyingi sana ikiwamo ile ya msokoto. Chumvi ya mawe na magadi ni biashara nyengine iliyokuwapo upande huo.
Upande wa Magharibi mwa soko kwa ndani, ni sehemu iliyokuwa ya kuuzia bidhaa kama mihogo, viazi vitamu na magimbi nk. Mmoja wa wazee maarufu mjini aliyekuwa akiuza viazi eneo hilo ni Hassan Masimenti, baba mzazi wa mchezaji mpira wa kimataifa wa zamani, hayati Jumanne Masimenti wa Simba, Cosmos na Taifa Stars.
Kwenye miaka ile hakukuwa na viazi mviringo au mbatata, kutoka Mbeya wala Arusha. Viazi hivyo vilikuwa havilimwi hapa nchini kabisa. Vilikuwa vikiagizwa kutoka Ireland, Ulaya; ndio maana vikapewa jina 'Viazi Ulaya’. Halikadhalika, vitunguu na tangawizi mbichi navyo vilikuwa havilimwi hapa nchini, bali navyo viliagizwa kutoka nje. ‘Viazi Ulaya’ na vitunguu, mara zote vilikuwa vikiuzwa kwenye maduka ya mitaani ya wahindi na washihiri.
Nyanya, ambazo siku hizo zilikuwa ndogondogo sana, zikiitwa tungule, mabamia, nyanya chungu, pilipili, ndimu; ukiwamo na ‘mchicha pori’, ni vitu vilivyokuwa vikipatikana katika sehemu hiyo ya mbogamboga.
Vitu kama karoti, spinachi, ‘hoho’, chainizi, ‘cauliflower’, ‘brocolli’ n.k, tulikuwa hatuvijui hata kazi yake nini, na kwa kweli vilikuwa havilimwi hapa nchini, ila kidogo tu, kwa ajili ya wazungu na wahindi. Hata hivyo, walikuwapo waswahili wachache waliokuwa wakitumia majani ya figiri kwa ajili ya kupunguza gesi tumboni.
Upande wa Barabara ya Nyamwezi kuelekea Tandamti ndiko kulikokuwa kunafanyika udalali wa bidhaa zote zinazoiingia sokoni hapo. Dalali Mkuu alikuwa ni Msaidizi wa Mkuu wa Soko (Assistant Market Master), Sherif Abdallah L’aatasi, huku Dalali Msaidizi akiwa Mzee Mshume Kiyate. Kazi ya kunadi bidhaa ilikuwa ikifanywa na Mzee Kiyate na Sherif L’aatasi yeye alikuwa akitoa stakabaadhi baada ya mnada na nyundo ya dalali kugongwa.
Baada ya kulipiwa kwenye chumba cha ofisi ya ‘Assistant Market Master’, iliyopo katikati ndani ya soko, bidhaa hutawanywa na kuuzwa kwa wanunuzi kwa matumizi ya nyumbani.
Katikati ya soko upande wa kushoto pembeni mwa ofisi hiyo ya malipo, kulikuwa na Ofisi ya Mkuu wa soko ambayo kwa muda mrefu soko lilikuwa likiongozwa na mpigania uhuru mashuhuri wa nchi hii hayati Abdulwahid Sykes.
Hayati Abdulwahid Sykes, alikuwa ni mtu aliyeheshimika sana mjini Dar es Salaam wakati huo kwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo kwenye African Association, Tanganyika African Association na baadaye (TANU), mpaka pale alipokuja kukabidhi kijiti kwa Mwalimu Julius.K. Nyerere mwaka 1954.
Marehemu Mzee Sykes, pia alikuwamo kwenye harakati za haki za wafanyakazi; Bodi ya elimu ya H.H. Aga khan, na ile ya taasisi ya Kiislamu ya Jamiatul-Islamia fi Tanganyika.
Uwepo wa ‘mashujaa wa Uhuru’ kama Mzee Mshume Kiyate, Abdulwahid Sykes na Sherif L’aatasi, unalifanya soko la Kariakoo kuingia katika moja ya sehemu muhimu sana katika historia ya kugombania uhuru wetu.
Mwl.Julius Nyerere wa Butiama pia alishawahi kuwa mwalimu wa sekondari pale Pugu wakati huo, alikuwa hapotei kila mwisho wa juma(weekend) kwenye soko hilo, kwani kila alipowasili mjini ni lazima apite ripoti kwa rafiki yake mkuu siku hizo, Abdulwahid Sykes pamoja na Mzee Mshume Kiyate, kupata maendeleo ya harakati za mapambano zinavyokwenda.
Pamoja na kwamba lilikuwa ni kosa kubwa kwa mfanyakazi kujihusisha na siasa, wazalendo wote hawa watatu walikuwa wakiuza, ndani ya ofisi zao pale sokoni bila woga na kificho hadi Chama cha TANU kilipoanzishwa mwaka 1954.
Ndani ya soko lile, kulia kulikuwa duka la vitabu lilojulikana kama Dar es Salaam Bookshop, ambapo kulikuwa kunauzwa vitabu mbalimbali vya kujisomea. Wazee wengi wa mjini waliweza kununua vitabu vya kujifunza kusoma vinavyoitwa “Someni kwa Furaha”, na kufundishwa na watoto wao nyumbani jinsi ya kusoma na kuandika. Kalamu za kuandikia za wino wa kuchovya za nibu, zikitumia wino wa ‘Quick ink’, na kalamu za wino za “TIKU” moja ya kalamu bora na ghali wakati huo pamoja na penseli ziliuzwa dukani hapo pia.
Kampuni ya magazeti ya Tanganyika Standard, ilikuwa na duka lake mahala hapo ikiuza magazeti ya aina mbalimbali pamoja na majarida kama vile magazeti ya DRUM, TIME na NEWSWEEK yaliyokuwa yakichapishwa Marekani.
Katikati ya soko pia kulikuwa na chumba cha redio. Maspika makubwa yalikuwa yametundikwa kila pembe ya soko kwa ajili ya nje ya soko ili watu wapate habari za siku pamoja na burudani.
Daima, usiku ulipokuwa umeingia sokoni Kariakoo huwapo watu wengi wakiwa wamekusanyika nje ya soko kwa ajili ya kusikiliza taarifa ya habari, vipindi vya mashairi ya kughani na kutumiana salamu kwa njia ya redio. “Tanganyika Broadcasting Corporation” (TBC), ilikuwa ndiyo stesheni pekee ya redio iliyokuwa ikisikika wakati huo kwenye miaka ya 1950s na 1960s. Nyuma ya jengo la soko, kwenye Barabara ya Mkunguni, kulikuwapo na ofisi ndogo ya Posta ya Kariakoo, ambayo wakati ule ilikuwa ndio posta pekee, si kwa watu wa Kariakoo tu, bali pia na Magomeni, Ilala, Msasani, Mtoni na kwengineko.
Ukiacha Posta hii ya Kariakoo, hakukuwa na ofisi nyengine tena mji mzima mpaka kule mjini Forodhani kwenye ile inayoitwa Posta ya Zamani. Pamoja na udogo wake, Posta ile ya Kariakoo, ilikuwa ndio tegemeo kubwa la watu kwa ajili ya kununua stempu, kupokea na kutuma barua, kupiga simu, kupeleka simu za upepo (telegrams) pamoja na kutuma pesa kwa ndugu na jamaa walioko nje ya mji huu. Mbele ya nyumba ile ya Posta, nje ya soko ukutani kulikuwa na tangazo kubwa la kipolisi lililosomeka: “CHUNGA BASKELI YAKO KWA TAHADHARI YA WEZI”.
Katika miaka ile ya ukoloni baiskeli ndio iliyokuwa nyenzo kubwa ya kusafiria kwa watu wa chini. Hivyo baskeli zilikuwa zinaegeshwa nyingi sana nje ya soko, jambo ambalo lilikuwa linasababisha wizi mwingi wa vipando hivyo. Tangazo jengine lilokuwapo hapo ni la kampuni inayotangaza ubora wa baiskeli ya “Raleigh”, ikiwahamasisha watu kununua baskeli hiyo ambayo picha yake kubwa ilitundikwa maeneo hayo.
Kule kwenye Barabara ya Tandamuti, ilikuwa ndiyo sehemu ya kuuzia nazi na minada yake. Ukielekea upande wa chini kabla hujafika Sikukuu Street, kulikuwa na duka kubwa na maarufu sana la viatu la BATA Shoes.
Duka hili lilikuwa maarufu sana kwa viatu vya raba na chacha (mithili ya yeboyebo), ambavyo ndio vilivyokuwa tegemeo kubwa kwa watu wenye kipato cha chini.
Kwa vile huu ulikuwa ni mji wa Waswahili, mahitaji mengine ya viatu yalipatikana kwa kutengenezesha makubadhi (viatu vya kufuma na kushonwa kiutamaduni) na Waswahili wa mwambao kwenye miji ya Dar es Salaam, Mombasa, Zanzibar, Lindi na Tanga.
Kwenye mtaa huohuo wa Tandamti ukivuka Sikukuu mkono wa kushoto, nyumba ya tatu ndio iliyokuwa ya Mzee Mshume Kiyate, aliyejitolea kwa hali na mali kwenye mapambano ya kulikomboa Taifa hili. Kuna wakati mtaa huu ulipewa jina la Mshume Kiyate, lakini baadaye kibao kikang’olewa na kurudisha jina la zamani la Tandamti.
Kwenye barabara hiyo ya Tandamti kona na Sikukuu, kulikuwa na kituo cha mafuta (Sheli) iliyokuwa ikimilikiwa na Muasia mmoja A. K. Nanji. Huyu alikuwa maarufu kwa sababu alikuwa na mabasi mengi sana ya kusafirisha watu kwenda maeneo ya mbali kama vile Kisarawe, Bagamoyo na Morogoro.
Kwenye Barabara ya Swahili na Mkunguni, nje ya soko la Kariakoo, zamani zile kulikuwa na stendi ya mabasi yaendayo maeneo ya Mtoni Kwa Azizi Ali, Mtongani hadi Mbagara.
Kwenye makutano ya Barabara ya Mkunguni /Nyamwezi kuna maduka mawili maarufu sana; moja ni lile la Shoto, ambalo limedumu mpaka leo kwa uuzaji wa sanda za kuzikia. Shoto mwenyewe alishafariki miaka mingi, lakini watoto wake wapo pale wakifanya kazi hiyo mpaka leo.
Ukitoka kwa kushoto, duka linalofuata ni la Nayani Bookshop, ambalo limekuwapo pale kwa takriban miaka 100 sasa, likiwa linauza vitabu mbalimbali vya dini na vya hadithi mbalimbali. Mbele ya duka hilo kwa mkono wa kushoto kuna jumba kubwa mithili ya godauni ambalo zamani lilitumika kama soko la chai.
Jumba la soko la chai limedumu pale kwa wakati wote huo likiwa lina mbao (mfano chai maharage) ambazo watu walikuwa wakitoa huduma ya chai kwa watu wenye shughuli sokoni na wale wanaofuata mahitaji yao. Kwa sasa biashara ya chai haipo tena mahala pale, na lile soko sasa limekuwa maarufu kwa kuuza vipuri chakavu vya magari pakijulikana kama Mnadani, Kariakoo. Mnada hasa ulikuwapo hapo ilipo Petroli stesheni ya Big Bon kwa sasa. Hayati Mzee Hamza Abeid Mwinyikondo wa Uweje, maarufu kama ‘Mzee Kumekucha’, wa Kumekucha Auction Mart; ndiye aliyekuwa dalali hapo mnadani miaka hiyo kabla ya uhuru. Mzee Hamza alikuwa akinadi vitu uwanjani hapo na yeye akipata kamisheni yake. Kutokana na uzoefu alioupata, serikali ya Tanganyika huru, ilimteua Mzee Kumekucha kuwa Dalali Mkuu wa Serikali, ambaye alizunguka nchi nzima kwenda kunadi vitu ambavyo serikali ilitaka vipigwe mnada.
Mkabala na Big Bon ya sasa, kulikuwa na Mzee mashuhuri sana wa Kimashomvi akiishi hapo akiwa na biashara yake ya kuuza mbao za kuzikia tu alijulikana kama Rajab Kiguu cha Mbuzi, ndo lilikuwa ndio jina lake. Ni mtu aliyeheshimika sana hapa mjini, kwa sababu alishirikiana vyema na watu wengine katika harakati za kijamii alizojiunga nazo kama vile Jamil- el -Manzil na siasa zilipoanza alishiriki pia.
Jumba la ghorora la Chaurembo, ambalo liko mkabala na Msimbazi Polisi, ndio kilichokuwa kituo kikubwa cha mabasi ya DMT— Dar es Salaam Motor Transport siku hizo, kwa mabasi yaendayo na kuingia sokoni kutokea Magomeni, Temeke, Ilala na Tom (sasa Posta).
Saidi Chaurembo, ndiye aliyelijenga jumba hilo wakati ule ambao waafrika wengi hawakuwa na uwezo wa kujenga nyumba kubwa kama ile.
Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo ni nduguye Saidi Chaurembo. Yeye alipata kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi katika jamii ikiwamo kuwa Imam Mkuu wa Msikiti wa Mtoro, mjumbe wa Maulid Committee na Kamati Kuu ya TANU Taifa. Pia kwa miaka kadhaa, amepata pia kuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kiislamu ya Aljamiatul- Islamia, iliyokuwapo pale Barabara ya New Street (sasa Lumumba).
Kwenye kona ya Barabara ya Tandamti/Kongo upande wa kulia kulikuwa na Duka la Poni (pawn). Hapo ni mahala ambapo watu walikuwa wakienda kuweka rehani vitu vyao na kukopeshwa fedha na mwenye duka kwa mkataba wa kulipa tarehe fulani. Sasa kitu chako hupigwa thamani na mwenye duka, na hivyo kuamua akupe kiasi gani.
Tarehe ya kurudisha ikifika kama hujaonekana, basi hutozwa faini na deni kuongezeka. Watu wengi sana waliweza kumaliza matatizo yao kwa namna hii, pamoja na kwamba biashara yenyewe haikuwa ikifanyika kihalali kabisa. Wapo waliosomesha Watoto, wapo waliojenga nyumba na kumaliza; wapo waliofanyia sherehe za harusi na unyago kwa watoto wao n.k.
Sasa, biashara hii ya poni ambayo ilienea kila mahala mijini waliokuwa wakiiendesha walikuwa ni Wahindi ambao walipata kibali hicho cha kuwanyonya wananchi kutoka kwa mtawalaMwingereza.
Serikali mpya ya kizalendo ilipoingia madarakani, moja ya vitu vya mwanzo kuvipiga marufuku ni hii biashara ya kudhalilishana ya Poni. Mabwana wakubwa wale Wahindi, walikuwa wanapenda kuletewa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na fedha ndio wakupe chochote.
Abeid Karume, baada ya mapinduzi matukufu kule Unguja, alizipiga marufuku taasisi pamoja na maduka ya Poni yaliyokuwa yamezagaa mjini Unguja na kuutangazia umma kwamba kila aliye na chake kwenye duka la poni aende akakichukue bure chini ya usimamizi wa Serikali ya Mapinduzi!
Sheikh Hassan Bakari ni kaka mkubwa wa Sheikh Muhiyidien Mkoyogole wa Temeke, na kiongozi wa Tariqa Qadiria. Yeye alikuwa na madrassa yake mahala hapo ambapo vijana wengi wa mjini walipitia kupata elimu ya Kiislamu. Tariqa Qadiria baadaye ilihamia kule Wailes, Temeke.
Kariakoo Pombe Shop, ni eneo lote lile lenye jumba la starehe la DDC. Pombe za kienyeji za kangara, chibuku, chimpumu na gongo zilikuwa zikiuzwa hapo kila wakati, huku harufu mbaya na moshi ikiwa ni kero kubwa sana kwa watu wa maeneo yale.
Baada ya uhuru kupatikana, Pombe Shop iliyokuwapo kwenye kona ya Kongo na Narung’ombe, ilivunjwa na kutengenezwa jengo lile zuri la DDC na Shirika la Maendeleo ya Dar es Salaam. Ilikuwa ni mahala hapohapo kwa mbele kidogo, ndipo zilipokuwa ofisi za magari ya abiria ya Muhindi mmoja Jamal Ismail, zilizokuwa zikifanya safari ya kwenda na kurudi Morogoro, Tanga na Moshi.
Mabasi mengine ni ya Champsi Mulji Babla na Abood Saleh Abood, maarufu Abood Bus, yaliyokuwa yakifanya safari ya kwenda Bagamoyo na Morogoro.
Hilo ndilo Soko la Kariakoo na mazingira yake lilivyokuwa kwenye miaka kabla ya Tanganyika kujitawala.
***
Kalamu ya mwandishi inaishia hapo Nakukumbusha kupitia ukurasa wetu kila siku saa 12 jioni ili uwe wa kwanza kuona mwendelezo wa similizi zetu.
Pia Kwa SHORT BACK STORIES Kama hii Naomba Tukutane Kila Jumamosi Saa 4 Asubuhi
MWISHO
Comments
Post a Comment